Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Jawadi Amuli katika moja ya darsa zake za maadili alizungumzia mada ya “Nafasi ya Madhehebu ya Ushia katika Historia ya Uislamu”, ambapo maudhui hii muhimu inawasilishwa kwenu wenye maarifa.
Alisema: “Ushia” si jambo lililozuka baada ya kuwepo kwa Amirul-Mu’minin Ali bin Abi Talib (as), bali ni ukweli uliojitokeza kabla ya yeye na sambamba na utume wa Mtume wa Uislamu (saw).
Swali kuu hapa ni: Je, “Ushia” kama mfumo ulianzishwa baada ya Amirul-Mu’minin au ulikuwa tayari upo kabla?
Jibu ni kuwa hapa tunakutana na maana mbili: Kwanza ni “mfumo wa Ushia (madhehebu ya Ushia)” na pili ni “kundi la Mashia.”
Mfumo wa Ushia uliibuka sambamba na kushuka kwa Qur'ani Tukufu, na mtu wa kwanza kuamini mfumo huu, kuutangaza na kuutetea alikuwa ni Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw).
Baada yake, alifuatiwa na Siddiqat Tahirah (sa), Amirul-Mu’minin Ali (as), na Ahlul-Bayt (as) wengine ambao wote walikuwa ni wafuasi na wasambazaji wa mfumo huu.
Hatua ya baadaye ilishuhudia kundi la watu wakijulikana kama Mashia, yaani watu waliomfuata Amirul-Mu’minin Ali (as). Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha kati ya "Mashia" kama kundi la kijamii na "Ushia" kama mfumo wa kiitikadi.
Mfumo wa Ushia umejengwa juu ya msingi kwamba walii wa Mwenyezi Mungu na mrithi wa Mtume lazima awe mtu mkamilifu na maasumu (asiye na dhambi wala makosa).
Mfumo huu unamwona Ali bin Abi Talib (as) na watoto wake walio maasumu (as) pekee kuwa ndio wanaostahiki cheo cha ukhalifa, kwa kuwa wao ndio mfano kamili wa ismah (maasumu) na ukamilifu wa mwanadamu katika mwendelezo wa risala ya Mtume.
Hivyo basi, Ushia si tu mwelekeo au mapenzi kwa Ahlul-Bayt, bali ni mfumo kamili wa maarifa na imani unaolinganisha daraja ya Uimamu na ile ya Utume, na kuiona kuwa ni mwendelezo wake halisi.
Mtume wa Uislamu (saw) alikuwa ndiye mtu wa kwanza kuamini wahyi wa Mwenyezi Mungu na akaamini utume aliokabidhiwa.
Vivyo hivyo, Amirul-Mu’minin Ali (as) alikuwa wa kwanza kuamini cheo chake cha wilaya na kuwa na yakini juu ya haki ya nafasi yake ya kiungu.
Imani hii ya ndani na yakini ndiyo nguzo kuu ya mfumo wa Ushia.
Kwa sababu hiyo, mwanzilishi wa kweli na muumini wa mwanzo wa mfumo wa Ushia ni Mtume Mtukufu (saw), na baada yake, Ahlul-Bayt (as) ni wahifadhi na wafasiri wa kweli wa mfumo huu.
Na kwa sababu hii, yeyote anayekataa wilaya ya Amirul-Mu’minin (as) na kutomtambua kuwa ni khalifa aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu, kwa hakika bado hajaamini ipasavyo katika risala ya Mtume; kwa kuwa katika madhehebu ya Ushia, Uimamu ni mwendelezo wa wahyi na risala, na ni sharti la ukamilifu wa imani.
Maoni yako